- Na Tom Lutali
Manchester United, almaarufu Red Devils, watakuwa wanazuru Stamford Bridge leo jioni kwa mechi inayosubiriwa kwa hamu na ghamu dhidi ya wenyeji Chelsea, yaani The Blues, ambao kwa sasa wako kileleni mwa ligi kuu ya Uingereza.
Red Devils wanasaka kurejesha hadhi yao ambayo ilididimia na kupelekea kutimuliwa kwa mkufunzi matata Ole Gunnar Solskjaer. Nafasi yake inashikiliwa kwa muda na mchezaji wa zamani na wa muda mrefu wa United, Michael Carrick, kabla ya Ralf Rangnick kutoka Barcelona kuchukua udhibiti rasmi.
https://pagead2.googlesyndication.com/pagead/js/adsbygoogle.js?client=ca-pub-2765037732072836Juma lililopita, United walifungwa 4-1 na limbukeni Watford, jambo ambalo lilitia msumari wa mwisho katika msimu wa Ole Gunnar. Hii ni baada yao tu kuraruliwa na majirani wao Manchester City na mahasimu wao wa jadi Liverpool.
Chelsea, kwa upande wao, wanatarajia kuendeleza msururu wa matokeo mazuri baada ya kuwafunga Leicester City 3-0 wikendi iliyopita. Kocha wa The Blues Thomas Tuchel amesema anatarajia mechi ya kusisimua.
“Mechi hii itakuwa ngumu sana ila kama viongozi,hatutaki kupoteza mechi yoyote kwa sasa,” alisema.
Timu hizi mbili zinakutana baada ya ushindi wao Jumanne katika kombe la Bara Ulaya (UCL). Manchester United waliwafunga Villarreal 2-0 huku Chelsea wakiwaadhibu Old Ladies Juventus 4-0.
Chelsea wanaingia katika mechi hii wakijua fika kwamba wapinzani wao wa karibu Liverpool walipata ushindi mnono wa 4-0 jana dhidi ya Southampton, tofauti kati yao ikiwa ni alama moja tu.
Katika mechi saba zilizopita wawili hawa wakikutana, Chelsea hawajapata ushindi wowote. Wametoka sare 4 na kupoteza 3.