Tija ya Mautuma: Kuku 600, vifaranga 400, hapa ni kazi tu!


Na Tom Lutali

Mwalimu Peter Simiyu ni mfugaji hodari wa kuku pale Mautuma. Kwa mbali, unapoingia katika lango lake, mlio wa kuku unakukaribisha; ishara kuwa kuna shughuli pevu inayoendelea huku. Tom Lutali amebahatika kuzungumza naye.

Je, nini kilichokuvutia na mradi huu wa kufuga kuku?

Nilianza na kuku 13 jogoo wawili na mwera 10. Hii kazi mimi mwenyewe niliipenda baada ya kugundua kuwa ina mapato mazuri, licha ya mimi kuwa mwalimu.

Tuelezee kuhusu safari yako ya ufugaji

Baada ya kugundua kuwa kuna changamoto za magojwa, nilianza kuweka mikakati ya kuzuia magojwa kwa kutafuta wataalamu na pia kukutana na wakulima wenzangu. Tuliunda kundi la WhatsApp ili kusaidiana kimawazo.

Kile kilinisukuma zaidi ni kuwa baada ya kuku kuwa wengi, watu walianza kuja kuwanunua kwa wingi na kuongeza kipato changu; ndipo nikagundua utamu wake. Nikaanza kupanua mbawa zaidi… Nimekuwa na kuku 400 ambao ni wa kienyeji na tayari wameuzwa wote. Kwa sasa nina kuku 600 na vifaranga 400 ambao ni wa Kizungu (Kenbrow ). Vifaranga hao niliwanunua Kisumu; unapowaona sasa wamekuwa sana kwa miezi miwili tu!

image
Mwalimu Simiyu akiwahudumia kuku wake.

Sadakta. Je, ni vipi mtu yafaa atunze kuku wake?

Kuku yafaa wapewe majani mabichi kama vile sukumawiki. Majani hayo unayafunga kwa mafungu na unayaning’iniza juu kuzuia uchafu na kinyesi kuchanganyika humo.

Chanjo kwa kuku pia ni lazima na iwe mara kwa mara. Mfano, kuku anapotaka kuanza kutaga, kuna kitu kinaitwa ” egg formula” hufanya yai kuwa la afya na kuzuia magojwa.

Kazi hii unaifanya pekee yako?

La hasha, jamii yangu wananiunga mkono asilimia mia kwa mia. Hata wakati ambapo nimeondoka utapata wamebadilisha maji na kusafisha mahali wanako kaa kuku na pia kuwapa chakula.

Usalama wa kuku wako unahakikisha vipi?

Usalama kwa kuku ni muhimu. Mimi nimewapa usalama wa kutosha– kwanza, nimewawekea ua ili kuwalinda dhidi ya mbwakoko na adui wake; pia nimeweka ‘net wire’.

Pahali pa kulala nimeweka pawe juu ya mbao ili kuondoa ubaridi. Umeme umo mle ndani pia kuhakikisha joto.

image
Ufugaji wa kuku una faida tele.

Changamoto zipi unazokumbana nazo katika ajira hii?

Kuku kama wanyama wengine changamoto hazikosi. Vyakula lazima ununue. Kuku pia wanahitaji utulivu; ukiwashtua wanapatwa na mzongo wa mawazo.

Unajivunia nini kutokana na mradi huu?

Kwa sasa, kuna mambo kadhaa najivunia kutokana na ufugaji wa kuku– nimefanikiwa kununua ng’ombe wa maziwa, nimekodi shamba la miwa na jamii yangu inapata cha kutia mdomoni kupitia miradi huu wa kuku.

image
Mwalimu Simiyu anajivunia faida za mradi wa ufugaji wa kuku.

Una malengo gani siku za usoni kutokana na mradi huu?

Sitarajii kuacha kazi hii kwa sasa ila nataka niipanue zaidi. Miaka kadhaa ijayo nataka niwe na mashine ya kusagia chakula cha kuku.

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.